
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho kuwa wanyenyekevu na karibu na wananchi, akisisitiza kuwa mamlaka waliyonayo ni dhamana ya muda.
Akizungumza leo Jumatano, Mei 28, 2025, jijini Dodoma, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo jipya la makao makuu ya CCM, Samia amesema viongozi hawapaswi kujiona juu ya wananchi kwa kuwa wao ndio wamiliki halali wa chama.
Rais Samia ameeleza kuwa historia ya CCM inaonyesha mabadiliko ya uongozi kwa nyakati tofauti, na hivyo hakuna kiongozi anayebaki milele, bali wote wanapita na kuacha nafasi kwa wengine kuendeleza pale walipoishia.
Ameongeza kuwa ni muhimu vijana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakalijua hilo na wote wakakakaa mguu sawa katika kukijenga chama hicho.
Rais Samia amesisitiza kuwa chama kinapaswa kuendelea kuwa nguzo ya wananchi katika kuamua hatima ya maisha yao na mustakabali wa Taifa, hivyo nidhamu, unyenyekevu na uadilifu kwa viongozi ni misingi isiyopaswa kubezwa.