
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanza kutekeleza mradi wa uchimbaji visima 52 katika Halmashauri nane za Mkoa wa Tabora ili kuwezesha wakulima wa maeneo hayo kuacha kulima kilimo cha mazoea cha kutegemea mvua na kujikita katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Katika Kijiji cha Miguwa, visima vitakavyochimbwa vitamwagilia zaidi ya ekari 1,590 na kuwafikia wakulima 1,567 ambao wengi wao wamekuwa wakitegemea mvua kwa ajili ya kilimo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo katika Kijiji cha Miguwa kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Katibu Tawala wa Nzega Mjini, Winfrida Funto amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwa nguvu katika kilimo cha umwagiliaji inalenga kuinua uchumi wa wakulima wadogo na kuongeza usalama wa chakula nchini.
Serikali kupitia Tume ya ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuchimba visima 67,500 katika Halmashauri 184 nchini ambapo zaidi ya wakulima 100,000 watanufaika moja kwa moja huku katika mwaka wa fedha 2025/2026 pekee, visima 1,300 vinatarajiwa kuchimbwa na Mkoa wa Tabora ukitarajiwa kupokea visima 52 katika Halmashauri nane ikiwemo Nzega Mjini.
Kazi ya uchimbaji visima hivyo katika Mkoa wa Tabora pekee imepangwa kutekelezwa ndani ya siku 21 na mradi huo unatarajiwa kuleta ajira za kudumu, fursa za kibiashara na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Mkurugenzi wa Uendelezaji Teknolojia, Mhandisi Naomi Mcharo amewaasa wananchi hao kulinda vifaa vinavyotumika katika mradi huo.
Mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji wa kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita kuleta mageuzi ya kweli katika sekta ya kilimo kupitia kilimo cha umwagiliaji.