Maelfu ya raia wamelazimika kukimbilia nchini Burundi, baada ya waasi wa M23 kuingia katika mji wa Uvira, Kongo.
Chanzo cha kijeshi na usalama kimesema waasi hao wameingia Uvira kupitia upande wa kaskazini mwa Burundi.
Haya yanajiri licha ya Marekani na mataifa kadhaa ya Ulaya kuwahimiza waasi wa M23, kusimamisha mara moja mashambulizi yao na kuitaka Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Uvira kudhibitiwa na M23 ni kitisho kikubwa cha kiusalama kwa Burundi, hasa ikizingatiwa kuwa mji huo upo ng’ambo ya Ziwa Tanganyika na kilometa chache kutoka mji mkuu wa kiuchumi wa Bujumbura.
Hata hivyo Burundi imeomba Balozi za nchi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa kuisaidia kutoa misaada ya chakula, malazi na matibabu ambapo mpaka sasa Burundi inawakimbizi zaidi ya laki moja (100,000) kutoka DRC ambao imekuwa ikihudumia kabla ya Uvira kutwaliwa na M23.