Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassa Ametangaza msamaha kwa wafungwa 1036 wa makosa mbalimbali katika maadhimisho ya miaka 64 ya uhuru wa Tanganyika.
Rais Dkt Samia ametumia Mamlaka yake chini ya Ibara ya 45(1)(a) – (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti.
Katika Msamaha huo wafungwa ishirini na mbili (22) wameachiwa huru leo Disemba 09, 2025 na wafungwa (1,014) wamepunguziwa adhabu zao na watabaki gerezani kuendelea kutumikia sehemu ya vifungo vilivyobaki.
Taarifa ya msamaha huo, imetolewa leo Desemba 09-2025 na Wizara ya Mambo ya Ndani na kutiwa saini na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene Mkoani Dodoma.
Waziri Simbachawene amesema Serikali inatarajia kuona wafungwa walioachiliwa huru leo wanarejea na kuungana na jamii katika ujenzi wa Taifa na kujiepusha na makosa yanayoweza kuwarejesha gerezani tena.
Hata hivyo maadhimisho haya ya miaka 64 ya uhuru yanafanyika bila sherehe kama ilivyozoelekea ,kutokana na kitisho cha Maandamano yasiyo na kikomo yaliyokuwa yakihamasishwa kufanyika siku ya Uhuru Desemba 09 mwaka huu.
Fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za uhuru zimeelekezwa kukarabati Miundombinu iliyoharibiwa kipindi cha maandamano yaliyozua vurugu wakati wa Uchagzui na baada ya Uchaguzi mkuu wa Rais wabunge na Madiwani Oktoba 29 2025.