
Wanafunzi wa darasa la tano na la sita katika shule ya msingi Mtakuja kata ya Lulembela wilayani Mbogwe mkoani Geita, wanalazimika kusomea chini ya miti kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Shule hiyo ina wanafunzi wapatao elfu 1 lakini vyumba vya madarasa havitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi.
Redio Kwizera imefika shuleni hapo na kuzungumza na wananchi pamoja na viongozi wa serikali ya kijiji ambao wamesema watoto wao wanapitia wakati mgumu hasa mvua zinaponyesha.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Mtakuja Bw. Abdalah Nkingwa amesema kutokana na changamoto hiyo, wananchi waliamua kujenga jengo lenye vyumba vitatu vya madarasa ambavyo vina zaidi ya miaka 6 bila kuezekwa.
Nkingwa amesema anasubiri nguvu ya serikali katika kufanya hatua za ukamilishwaji wa jengo hilo ili wanafunzi wapate mahali pazuri pa kusomea.
Licha ya uhaba wa vyumba vya madarasa, shule hiyo pia ina changamoto ya vyoo, ofisi ya walimu pamoja na uhaba wa walimu huku wananchi wakieleza uhaba huo unatokana na mazingira yasiyo rafiki.
Redio Kwizera imemtafuta Afisa Elimu Msingi wilaya ya Mbogwe Bw. Emmanuel Mayala na ameiambia Radio Kwizera kuwa, hawezi kuliongelea suala hilo kwani lipo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri.
Aidha jitihada za kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbogwe bado hazijafanikiwa kutokana na simu yake ya mkononi kutokupatikana hewani.