
Wakazi wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera wameadhimisha miaka 61 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao.
Akiongoza zoezi hilo la usafi wa mazingira ambalo limefanyika leo hii Aprili 26 mwaka huu katika Kata ya Muleba Katibu Tawala Wilaya ya Muleba, Bw. Benjamini Mwikasyege amesema kuwa kuna haja ya kuendelea kuenzi na kuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama walivyofanya viongozi waliotangulia.
Bw. Mwikasyege amesema kuwa tangu uwepo muungano pamekuwa na maendeleo makubwa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo ni Afya, Maji, Barabara na Umeme hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kuendelea kuenzi muungano kwani ndio tunu ya taifa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Muhaji Bushako amesema watahakikisha wanahamasisha wananchi wanaendeleza zoezi la usafi wa mara kwa mara kwenye maeneo yao badala kufanya kwenye matukio maalum pekee.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Isaya Mbenje amewataka wakazi wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili ambalo linatarajia kuanza may mos kwaka huu.
Aidha Tangayika na Zanzibar ziliungana kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania April 26 mwaka 1964 chini ya viongozi hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Hayati Abeid Aman Karume ambapo kwa siku ya leo Muungano huo umefikisha miaka 61.