
Jeshi la polisi kitengo cha polisi jamii Wilayani Biharamulo mkoani Kagera limewataka wananchi kuendelea kuhamasisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi kuelekea uchaguzi mkuu wa Mwezi October.
Mratibu mkuu wa kitengo hicho wilayani humo SP. Paschal Kiula ameeleza hayo wakati akizungumza na wananchi kuhusu umuhimu wa wao kushirikiana na Polisi katika ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya jamii.
Kiula amesema wananchi wana fursa ya kulinda na kutunza amani kabla na baada ya uchaguzi na kuepuka waasi wanaoweza kuivuruga nchi na kuwataka wananchi kutoa taarifa za watu wenye viashiria vya kusababisha vurugu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mkuu wa polisi wilaya ya Biharamulo ASP. Charles Kidesheni amesema jeshi la polisi litakuwa karibu na wananchi kwa kuzingatia viapo vyao vya kulinda usalama wa raia na mali zao hali ambayo itaisaidia kuimarisha usalama wao.