
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, inatarajiwa kuupokea Mwenge wa Uhuru kimkoa Agosti 3, 2025 katika viwanja vya kituo cha mabasi Kagongwa majira ya saa 12 kamili alfajiri ukitokea mkoani Tabora.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu, amesema Maandalizi ya kupokea mwenge wa uhuru yanaendelea ikiwa ni pamoja na viongozi na watumishi wa Serikali kuendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo itakayofikiwa na mwenge.
Aidha Kibetu amesema, miradi 7 yenye zaidi ya Shilingi Bilioni 6.4 itapitiwa na mbio hizo ambapo mradi 1 utakabidhiwa kwa kikundi cha vijana cha madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) 10, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 110 pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la uraibu wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama wa zaidi ya Shilingi milioni 349.8 unatarajiwa kuwekwa jiwe la msingi
Hata hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru kwani watapata fursa ya kuukimbiza na kuangazia miradi yao ya maendeleo iliyolenga kuwasogezea huduma karibu.