
Waziri wa Maji, Juma Aweso, amepiga marufuku matumizi ya wasoma mita wa mtaani (vishoka) katika mamlaka zote za maji nchini, kufuatia ongezeko la malalamiko kutoka kwa watumiaji kuhusu kubambikiziwa ankara za maji.
Akizungumza Mei 28, 2025 katika kikao kazi cha mameneja na wakurugenzi wa mamlaka za maji kinachofanyika jijini Mbeya, Waziri Aweso amesema hatavumilia viongozi wa mamlaka watakaoshindwa kushughulikia kero hizo.
Amesema kuwa licha ya Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maji nchi nzima na kupunguza kero ya upatikanaji wa huduma hiyo, bado huduma kwa wateja imeendelea kuwa changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa kwa nguvu zote.
Ameeleza kuwa Serikali imepanga suluhisho la kudumu kwa kuanzisha mfumo wa usomaji mita unaoendana na matumizi halisi ya maji ya mteja, ili kuondoa malalamiko ya bili zisizo sahihi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ameonya mamlaka zote zinazowaajiri wasoma mita na watoa huduma walioko nje ya mfumo rasmi (vishoka), kwani wamekuwa wakisababisha gharama kubwa za uendeshaji, kuunganisha maji kiholela mitaani na kuziba mivujo wanayoisababisha wao wenyewe.
Kikao hicho kazi kimehudhuriwa na mameneja wa huduma kwa wateja na wakurugenzi kutoka mamlaka za maji nchini kote.