
Watu watatu wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu katika halmashauri ya mji wa Kasulu Mkoani Kigoma kwa kipindi cha kuanzia Agosti 21 hadi Septemba 3 mwaka huu.
Akisoma taarifa ya hali ya maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu Kwenye kikao cha kamati ya afya ya msingi PHC halmashauri ya Mji wa Kasulu Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kasulu Bw.Sabato Kwizera ameitaja idadi ya wagonjwa 24 kuripotiwa katika hospitali ya mji Wa Kasulu Mlimani na kituo cha afya kata ya Nyansha na kusababisha vifo vya watu wa tatu kwa kipindi cha wiki mbili pekee.
Mratibu wa Huduma za Afya Halmashauri ya mji Kasulu Dkt Kazimoto Sangwa amesema baadhi ya wanajamii wamekuwa na imani potofu kuwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hutokea msimu wa masika pekee jambo ambalo limepelekea baadhi yao kushindwa kufika hospitali kwa wakati huku akizitaja kata Nyasha na Kigondo kuwa na idadi ya kesi nyingi za wagonjwa wa Kipindupindu
Mwakilishi kutoka ofisi ya Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma dkt Hosea william ameshauri jitihada za makusudi kufanyika kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa huo unadhibitiwa kabla ya masika kuanza.
Katika kikao hicho maadhimio mbalimbali yamefikiwa ikiwa ni pamoja na wataalamu wa afya kutoa elimu kwa umma Lengo ikiwa ni kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wengi katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Mwakilishi kutoka wizara ya Afya Makao makuu Dodoma Dkt Frank Jacobo ametoa msisitizo kwa watumishi wa halmashauri ya mji wa Kasulu kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa.