Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa gari la wagonjwa (ambulance), tukio lililotokea Oktoba 25, 2025 katika Manispaa ya Musoma.
Watuhumiwa hao ni Goodluck Chacha (26) dereva na mkazi wa Tarime mkoani Mara, Karume Kihedu (26) fundi magari na mkazi wa Arusha, Said Ramadhani (39) fundi magari na Elias Joackim (53) wote wakazi wa Arusha.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo na mashtaka yao kusomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Hadija Masala ambaye alimtaka Wakili wa Serikali Michael Kayombo kuwasomea mashtaka na kuwataka washtakiwa kutojibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Kayombo amesema kuwa mashtaka wanayowakabili washtakiwa ni ya Uhujumu Uchumi na kuongoza genge la uhalifu na wizi huku akibainisha kuwa uchunguzi bado unaendelea na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Hadija ameiahirisha kesi hiyo hadi Februari 25, 2026 ambapo itasomwa tena na watuhumiwa wote wamerudishwa rumande.
