
Wazazi ambao watoto wao wanakwenda kusoma nje ya nchi kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 wametakiwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa watoto wao kitaaluma na tabia.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel alipokutana na wazazi na wanafunzi hao siku ya Jumapili kwenye ofisi za GEL jijini Dar es Salaam ambapo wazazi na wanafunzi hao walipewa taratibu za mambo ya kuzingatia kabla, wakati na baada ya kufika nchi wanazokwenda.
Katika mkutano huo, ambao ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani, wanafunzi wengi walikabidhiwa viza zao tayari kwa ajili ya safari ya kuelekea vyuoni, huku wazazi wakipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana baadhi ya wawakilishi wa vyuo hivyo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema wazazi wanapolipa ada wasidhani kwamba wamemaliza jukumu lao na badala yaake bado wanakuwa na wajibu wa kuwafuatilia.
Alisema ni muhimu sana kila mzazi akafanya hivyo ili kujua maendeleo ya mtoto wake kitaluma na tabia anapokuwa chuoni kwani baadhi yao wamekuwa wakibadilika na kufanya mambo yasiyostahili na kushindwa kuhitimu.
Mollel alisema ataendelea kutekeleza wajibu wake kuhakikisha kila mwanafunzi aliyekamilisha taratibu anafanikisha safari yake ya kwenda kuanza masomo katika vyuo walivyodahiliwa kwa wakati.
Alisisitiza kuwa maslahi ya mwanafunzi ndiyo kipaumbele cha kwanza na kwamba hatakubali kuona chuo chochote kinashindwa kutimiza wajibu wake.