Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwamba ifikapo mwisho wa Februari 2026 awe amefikisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata Magharibi, kutokana na hali mbaya ya madarasa matatu ambayo hayatumiki kwa sasa.
Amesema hayo leo Februari 13, 2026, katika ziara yake mkoani Tanga alipokuwa akiweka jiwe la msingi na kukagua kituo cha kupoza umeme Mkata, ambapo awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkata Magharibi, Mussa Ngana, aliibua hoja ya uchakavu wa madarasa ya shule hiyo.
Ngana amesema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 1,000 na ina madarasa manne yanayotumika, huku mengine matatu hayatumiki, na mhandisi akikataza matumizi yake pamoja na nyumba ya mwalimu kutokana na uchakavu.
Aidha Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, amewaelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Vijijini na Katibu Mkuu wa wizara yake kila mmoja kupeleka Sh50 milioni katika shule hiyo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mengine mapya.
” Profesa Shemdoe Shule hii ipo Mkata Magharibi, miaka miwili iliyopita tuliteta pesa ambayo imemalizia ujenzi wa shule mpya ya Julius Nyerere yenye madarasa 14, na tayari kuna wanafunzi wanasoma pale ambao ni 670,” amesema.
