
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Kanda ya Victoria, Mbunge Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho Bw. Ezekia Dibogo Wenje ametangaza kukihama Chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM, akisema “Kwa miaka 15 iliyopita nimekuwa Ligi daraja la Kwanza na sasa nimeamua kujiunga na Ligi Kuu.”
Wenje ametangaza maamuzi hayo leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 kwenye Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Chama Hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chato Mkoani Geita na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Asharose Migiro, akimpongeza pia Dkt. Samia na Chama Cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia amani na utulivu wa Tanzania suala ambalo limewezesha upigaji wa hatua kubwa za maendeleo na ustawi.
Akieleza imani yake kuwa Taifa ni kubwa kuliko mtu ama taasisi yoyote ndani ya nchi, Wenje pia ameonesha masikitiko yake kwa kile kinachohamasishwa kuelekea Oktoba 29, 2025, akisema maandamano hayo yanaandaliwa na watu ambao hawapo Tanzania wao na familia zao, akiwataka Watanzania kutafakari kwa kina kuhusu suala hilo la maandamano, akitolea mfano wa simulizi za Kiongozi wa dini aliyefahamika kama Kibwetere, aliyehamasisha waumini wake kuuza mali zao na baadae kuwachoma moto kwa madai ya kuwapeleka mbinguni huku yeye akijiweka kando na matendo hayo.
Aidha Wenje ameeleza pia kuhusu madai kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM imekizuia Chadema kushiriki uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema maamuzi ya Vikao vya Chama hicho pamoja na kuhofia kushindwa vibaya dhidi ya Chama Cha Mapinduzi ndiyo yaliyokiondoa Chama hicho kuweza kushiriki katika uchaguzi Mkuu ujao.
“Tarehe 20 Januari mwaka huu tulikutana tukafanya kitu kinaitwa Baraza kuu la Chama. Baraza likatoa mapendekezo tukapeleka kwenye Mkutano Mkuu wa Chadema, wote tukakubaliane Chadema hatushiriki Uchaguzi.Tulishauriwa mpaka na wazee wa maana duniani akiwemo Raila Odinga naye, akawaambia duniani hapa wampe mfano wowote Afrika wa Chama ambacho kiliwahi kususia uchaguzi halafu bado kikaendelea kuwepo.
Kwahiyo Mhe. Rais mimi nimechoka kukunja ngumi na kwa miaka 15 nimekuwa kwenye ligi daraja la kwanza na leo nimeamua kuja”