Na Samwel Masunzu- Kibondo, Kigoma
Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) limeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kilimo Tija Kigoma KITIKI unaotekelezwa mkoani Kigoma.
Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri nne za mkoa wa Kigoma ambazo ni Kasulu vijijini, Kasulu mji, Kibondo na Kakonko ukisimamiwa na shirika la WFP na kutekelezwa na mashirika mengine ambayo ni World Vision Tanzania pamoja na Good Neighbors Tanzania.
Akiwa kwenye maadhimisho ya siku ya wakulima kwenye kijiji cha Katanga wilayani Kakonko mkoani Kigoma na kukagua shamba darasa la kikundi cha Kwizera, Meneja mradi wa KITIKI kutoka shirika la WFP – Kasulu Bw. Hyoyedl Lee Amesema shirika linaridhishwa na namna ambavyo mradi huo unatekelezwa.
Hyoyeld Lee amesema shirika la WFP limekuwa likishirikiana na wadau wengine ikiwemo serikali ya Tanzania, wauzaji wa pembejeo za kilimo,wazalishaji na wasambazaji wa mbegu ili ziweze kuwafikia wakulima.

Mwakilishi wa Meneja wa mradi huo kutoka shirika la World Vision Tanzania mkoa wa Kigoma Bw. Samson Katabila amesema shirika limekuwa likitoa elimu kwa wakulima kuhusu namna bora ya kuongeza uzalishaji na kuepuka upotevu wa mazao.
Amesema wakulima kupitia mradi wanapata pembejeo za kilimo pamoja na mbegu bora zinazoleta tija kwa wakulima tofauti na mbegu ambazo walikuwa wakizitumia.
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima cha Kwizera –Katanga Bw. Yusufu Ngaye ameyashukuru mashirika yanayotekelea mradi huo kwa kuwapatia elimu ya kilimo na pembejeo za kilimo hali ambayo imeongeza uzalishaji tofauti na kilimo kilichozoeleka.
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo, Diwani wa kata ya Katanga Bw. Ezekiel Bikata amewaasa wakulima waliopata elimu kupitia mradi huo, kuendelea kutumia elimu hiyo katika uzalishaji wa mazao na elimu hiyo isiishie kwenye vikundi, bali iwe chachu kwa jamii nzima.
Mradi wa kilimo Tija Kigoma KITIKI ulianza mwaka 2023 ukitekelezwa na mashirika ya World Vision Tanzania na Good Neighbors Tanzania yakisimamiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP kwa ufadhiri kwa serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika lake la Maendeleo KOICA.
