Clement John- GEITA
Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ameagiza Watumishi wa Umma na wadau wengine kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka 10 inayotarajiwa kutolewa kwenye Mikoa 7 Kanda ya ziwa.
Komba ametoa agizo leo kwenye kikao cha PMC na Watumishi hao kilicholenga kuongeza hamasa kwa wazazi na walezi pamoja na elimu kuhusu chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka 10 kupitia Viongozi wa dini, Serikali na wadau wengine.

Amesema chanjo hiyo ni salama na wananchi wanatakiwa kupuuza taarifa potofu kuhusu chanjo hiyo kutokana na usimamizi madhubuti wa wafadhili wa chanjo hiyo ikiwemo Shirika la Afya duniani (WHO), UNESCO, na Shirika la RED CROSS.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt Omary Sukari imeeleza kuwa chanjo hiyo ya polio inatarajiwa kuwafikia zaidi ya watoto milioni 1 na laki 1 mkoani Geita na zaidi ya watoto milioni 6 watafikiwa kwenye Mikoa 7 Kanda ya ziwa.
Mratibu Msimamizi wa huduma za chanjo Mkoa wa Geita Bi. Wille Luhangija amesema chanjo hiyo itafanyika kwenye mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Singida, Mara, Simiyu na Tabora kuanzia Machi 24 mpaka 27 mwaka huu na awamu nyingine itakuwa mwezi mei mwaka huu.
Kampeni hii imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kudhibiti ugonjwa huo kufuatia kuibuka kwa vimelea vyake Mkoani Mwanza.
