SOMALIA: Ndege ya raia iliyokuwa na watu 55 imetua baharini karibu na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde mjini Mogadishu baada ya rubani kufanya uamuzi huo kufuatia hitilafu ya kiufundi.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia kupitia mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Ahmed Macalin Hassan imesema ndege hiyo ilipaa kutoka Mogadishu kuelekea Galkayo, mji mkuu wa mkoa wa Mudug, wakati hitilafu iliporipotiwa muda mfupi baada ya kupaa na marubani waliomba kurejea.

Vikundi vya kutoa msaada vilitumwa mara moja, na watu wote 55 walihamishwa hadi eneo salama. Hakuna vifo au majeraha makubwa yaliyoripotiwa.
Shirika la ndege, Starsky, lilisema limeanzisha uchunguzi kuhusu tatizo la kiufundi na kupongeza uamuzi wa kijasiri wa rubani kutua karibu na bahari, huku maafisa wa usafiri wa anga wanasema uchunguzi zaidi unaendelea.
