Na Michael Mpunije- Buhigwe, Kigoma
Wakazi wa kitongoji cha Janda Juu kata ya Janda wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wamejitolea kutengeneza Barabara itakayowasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani pamoja na kusaidia wakazi wa eneo la Kilulu kupata huduma mbalimbali kwa urahisi ikiwemo Elimu na huduma za afya.
Wakizungumza wakati wa zoezi la utengenezaji wa barabara hiyo, baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho akiwemo Joseph Chiha na Angela Kassim wameeleza kuwa ukosefu wa barabara hiyo umekuwa changamoto kubwa inayokwamisha upatikanaji wa huduma muhimu hususani kwa wakazi wa eneo la Kilulu ndani ya kitongoji hicho.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Janda Juu, Damas Lugigidi amesema kuwa juhudi za wananchi kujitolea kutengeneza Barabara hiyo zinaonesha namna walivyo tayari kushirikiana katika kuleta maendeleo ya eneo lao, huku akiiomba serikali kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha barabara hiyo inaboreshwa zaidi na kudumu kwa muda mrefu.
Aidha Diwani wa kata ya Janda Wilayani Buhigwe Shabani Seleman amesema kuwa ameshawasilisha changamoto ya Barabara hiyo katika mamlaka husika ili kuona uwezekano wa kutengenezwa kwa kiwango bora ili kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.

