Na William Mpanju- Biharamulo, KAGERA
Timu ya mpira wa miguu ya Jeshi la Polisi Kituo cha Biharamulo mkoani Kagera imeibuka mshindi wa michuano ya ligi ya maadhimisho ya Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, baada ya kuifunga timu ya Bodaboda kwa mikwaju ya penalti 5–4.
Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa CCM Biharamulo ulimalizika kwa sare ya bao 1–1 ndani ya dakika 90, kabla ya kuamuliwa kwa penalti ambapo timu ya Polisi iliibuka kidedea kwa mikwaju ya penalti 5–4.

Baada ya mchezo huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Biharamulo, Kasimu Kirondomara, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya SACP Advera Bulimba ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliikabidhi timu ya Polisi mbuzi mmoja kama zawadi ya ushindi, huku timu ya Bodaboda iliyoshika nafasi ya pili ikipewa mbuzi mdogo.
Amesema mashindano hayo yamekuwa na lengo la kuimarisha upendo, amani na mshikamano miongoni mwa jamii, akisisitiza kuwa michezo ina nafasi kubwa katika kuunganisha watu na kuimarisha afya.
Kaulimbiu ya mashindano hayo imeendelea kuakisi umuhimu wa michezo katika jamii, ikibeba ujumbe kuwa mpira ni afya na mpira ni upendo.

