MITI 30 imepandwa katika Shule ya Msingi Mnanzi Mmoja kati ya miti 3,850 iliyopandwa nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
Tukio hilo la upandaji miti limefanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana Juni 28, 2026 katika shule hiyo iliyopo Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.
Akizungumza, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema lengo la shughuli hiyo ni kuacha urithi kwa vizazi vijavyo na kuwafanya watoto watambue kuwa miti hiyo imepandwa kwa gharama zinazotokana na kodi zinazolipwa na wazazi wao.
Amesema hatua hiyo inalenga pia kuwahamasisha watoto kuwa walipakodi wa baadaye, huku akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni sehemu ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa endelevu.
“Tunataka watoto waliopo hapa na watakaokuja baadaye wakumbuke kuwa TRA ilipanda miti kwa gharama ambazo ni kodi za wazazi wao. Pia wahamasike kama wazazi wao walivyolipa kodi, na wao waje kulipa kodi,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa wamefanya hivyo nchi nzima kwa miti 3,850, huku miti 30 ikipandwa katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja na kutarajiwa kuanza kuzaa matunda baada ya miaka miwili.
Amesema TRA imeahidi kugharamia utunzaji wa miti hiyo hadi itakapoanza kutoa matunda,na wanafunzi watakaoshiriki kuilinda watapatiwa token na mwalimu naye akipata fedha kila mwezi kwa kipindi cha miezi 12 kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
“Ili nchi iendelee na iwe kama ilivyo, lazima tulinde mazingira, na mazingira ni miti. Lakini haiwezekani bila kulipa kodi, hivyo uwajibikaji huo ni sehemu ya kuhamasisha watoto kuona umuhimu wa ulipaji wa kodi unaofanywa na wazazi wao,” amesema.
