Kabla ya kuwa sauti kubwa Kanda ya Ziwa, Radio Kwizera ilikuwa ndoto kubwa iliyoanzia Ngara!

Picha hizi ni sehemu ya historia, ni kumbukumbu za mwanzo wa safari ya taasisi ambayo leo imekuwa miongoni mwa majina yenye heshima kubwa katika tasnia ya utangazaji nchini Tanzania.
Tarehe 12 Agosti 1995, Radio Kwizera ilianza kurusha matangazo yake rasmi mjini Ngara, mkoani Kagera, ikiwa imeanzishwa na shirika la Jesuit Refugee Service (JRS), kwa kushirikiana na wadau wa huduma kwa wakimbizi.
Wakati huo, lengo lilikuwa zaidi ya kurusha matangazo. Ilikuwa ni kuunganisha jamii, kutoa taarifa sahihi, kuelimisha na kujenga amani na maridhiano kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, hususan kutoka Rwanda na Burundi.

Lakini miaka ilivyokwenda, historia ikaandika ukurasa mwingine mkubwa! Kutoka kwenye studio za mwanzo zilizokuwa na vifaa vya teknolojia ya wakati huo.
Radio Kwizera imepitia mageuzi makubwa ya kiteknolojia, kiutendaji na kiuhudumiaji. Kutoka Ngara, mawimbi yake yameendelea kuvuka mipaka, kufikia mamilioni ya watu ndani na nje ya Tanzania.
Radio Kwizera si kituo cha redio kinachojivunia miaka mingi ya uwepo wake pekee. Ni taasisi ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa sehemu ya malezi ya vipaji, kukuza uwezo na kuandaa wataalamu wa tasnia ya habari na utangazaji.
Ndani ya historia yake, kuna watangazaji, waandishi wa habari, watayarishaji wa vipindi na wataalamu wa maudhui ambao wamepitia katika mikono yake, kujifunza, kukua na kuendelea kung’ara katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Kwa maneno mengine, Radio Kwizera haijawa ikitoa matangazo pekee; imekuwa ikizalisha watu wanaokwenda kuifanya tasnia ya habari izidi kukua!

Hiyo ndiyo tofauti ya taasisi yenye uzoefu na taasisi yenye historia. Leo, tunapozungumzia Radio Kwizera, tunazungumzia zaidi ya miaka 31 ya uzoefu, uaminifu, ubunifu, huduma kwa jamii na mchango katika maendeleo ya tasnia ya habari.
Tunazungumzia kituo kinachofikia wasikilizaji Kagera, Kigoma, Geita, Mwanza, Shinyanga na maeneo mengine, huku mawimbi yake yakivuka mipaka ya Tanzania na kuwafikia wasikilizaji Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kutoka redio ya jamii hadi kuwa jukwaa kubwa la matumaini, Kutoka studio za mwanzo hadi ulimwengu wa kidijitali, Kutoka kizazi kimoja cha watangazaji hadi kizazi kingine.
Ndiyo maana tunasema: Radio Kwizera ni zaidi ya redio. Ni shule, ni historia, ni uzoefu na ni taasisi iliyoweka alama yake katika tasnia ya utangazaji!
Na ndiyo maana bado tunasimama kifua mbele na kusema:
RADIO KWIZERA- RADIO NAMBA 1 KANDA YA ZIWA! Jukwaa la Matumaini. Tangu 1995.

Je, unamkumbuka mtangazaji gani aliyepitia Radio Kwizera na baadaye kuwa jina kubwa katika tasnia ya habari Tanzania? Na wewe ulianza kuisikiliza Radio Kwizera mwaka gani?
Historia hii isibaki kwenye picha pekee. Isambaze ili kizazi cha leo kijue tulikotoka!
