Na Shafiru Yusuph- Muleba, KAGERA.
Wananchi wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wametakiwa kuacha tabia ya kuvamia na kujenga katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga, amesema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya barabara ya lami yenye urefu wa mita 550 kwa wakazi wa Kitongoji cha Bukono, Kata ya Muleba iliyojengwa na ndugu Moses Kiduduye.
Dkt. Nyamahanga amesisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo bila vikwazo ikiwemo barabara.

Awali akisoma taarifa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini Muhandis Dativa Telesphory amesema Barabara hiyo yenye urefu wa mita 550 na inatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Kitongoji hicho.

