Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa majibu makali mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), ikiyashutumu mataifa ya Magharibi na asasi za kimataifa kwa kutoa kauli za upendeleo na “kuchagua matukio” kuhusu hali ya usalama nchini kufuatia uchaguzi wa Oktoba 2025.
Katika haki yake ya kujibu iliyotolewa Machi 2, 2026, Tanzania kupitia kwa Mwakilishi wake wa Kudumu katika Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) mjini Geneva, Dk. Abdallah Saleh Possi, amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia haki yake ya kujibu kauli zilizotolewa na wawakilishi wa Ubelgiji, Uingereza, Uswisi, Sweden, Ireland, Ubelgiji, Norway, Jumuiya ya Ulaya (EU), pamoja na mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International.
Tanzania imepinga vikali madai ya mauaji ya kinyume cha sheria yaliyotolewa na Uingereza, ikidai kuwa washirika hao wa kimataifa wamefumbia macho uharibifu mkubwa uliofanywa na vikundi vilivyohamasisha vurugu huku Serikali ikieleza kuwa tarehe 29 Oktoba 2025, nchi ilishuhudia vitendo vya kigaidi vilivyolenga vituo vya polisi, ofisi za serikali, na miundombinu ya umma.
Tanzania imesisitiza kuwa kama nchi huru, ina jukumu la kikatiba la kulinda utulivu wa umma na kwamba hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama zilikuwa ndani ya wigo wa sheria ili kuzuia nchi isiingie kwenye ghasia.
Serikali imewataka washirika wa kimataifa kuheshimu uhuru wa nchi na kutozichukulia hatua za kulinda amani kama ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kuhusu shinikizo la kufanya uchunguzi huru, serikali imekumbusha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishateua Tume Huru ya Uchunguzi kisheria ambapo Tume hiyo imepangiwa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake tarehe 3 Aprili, 2026.
