Kijana Baisi Sadam Nyangali, ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji (dancers) wa Misso Misondo, amefariki dunia jana baada ya kuhusika katika ajali ya gari.
Taarifa ya kifo chake imetolewa na Misso Misondo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akieleza masikitiko makubwa kufuatia kumpoteza mmoja wa watu waliokuwa sehemu muhimu ya safari ya kundi hilo.
Marehemu Baisi alikuwa miongoni mwa vijana walioanza kufanya kazi na Misso Misondo tangu kuanzishwa kwa kundi hilo. Alijizolea umaarufu kutokana na uwezo wake wa kucheza na uhodari wake jukwaani, hali iliyomfanya kupendwa na watu wengi.
Kifo cha Baisi kimeacha pengo kubwa kwa familia yake na katika tasnia ya burudani, hususan kwa wenzake waliokuwa wakifanya naye kazi kwa karibu. Tunatoa pole kwa familia ya marehemu, Misso Misondo, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
