Miss World Tanzania 2026, Latricia, amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris, ambapo wamejadili nafasi ya vijana katika kuitangaza Tanzania kupitia utamaduni, utalii na lugha ya Kiswahili.
Latricia yupo nchini Ufaransa kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, yanayofanyika kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali. Maadhimisho hayo yanalenga kukuza matumizi ya Kiswahili duniani na kuimarisha diplomasia ya utamaduni.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Saidi Othman Yakubu alimpongeza Latricia kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa vijana kutumia ushawishi wao kuitangaza lugha ya Kiswahili, utamaduni na vivutio vya utalii vya Tanzania.
Kwa upande wake, Latricia amesema ataendelea kuwa balozi mwema wa Tanzania kwa kuitangaza nchi kupitia utamaduni, utalii na lugha ya Kiswahili, huku akihamasisha watu wengi zaidi duniani kujifunza na kutumia Kiswahili.
