Walei na waamini wote Jimbo Katoliki la Geita wameaswa kutoa ushirikiano kwa Mapadre ili kuongeza ufanisi katika utunzaji wa mali za Kanisa na utekelezaji wa huduma za kichungaji jimboni humo.
Rai hiyo imetolewa na Mhashamu Askofu Flavin Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita katika homilia yake mapema leo wakati wa Ibaada ya Misa takatifu ya kupewa Daraja takatifu la Upadre kwa Mashemasi 8 kutoka Parokia 7 za Jimbo hilo.
Mhashamu Askofu Kassala amesema kuwatunza Mapadre ni jukumu la Walei na kwamba kutekelezwa kwa jukumu hilo ni kutengeneza mazingira rafiki katika uratibu wa shughuli za kichungaji kwenye maeneo yao.
Mapadre hao wapya kupitia kiapo chao cha Kumlinda Mtoto wameahidi kutekeleza wajibu na majukumu watakayopangiwa kwenye maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Geita.
Mkurugenzi wa Miito Jimbo Katoliki la Geita Padre Michael Fikiri amehimiza wazazi na walezi kupeleka watoto wao katika wito wa Upadre ili kuongeza watumishi kwenye huduma za kichungaji jimboni humo.
Mashemasi 8 waliopewa Daraja takatifu la Upadre ni Abel Nzobe wa Parokia ya Bikra Maria Mama wa Mungu Nyehunge, Caston Isengwa wa Parokia ya Mt. Yakobo Mkuu Mwangika, Deogratius Ng’webeya wa Parokia ya Mt. Rita wa Cascia Kharumwa, Dickson Manimba wa Parokia ya Mt. Paul Mtume Mwatulole, Frank Tiganyilana wa Parokia ya Bikra Maria Msaada wa Daima Kome, Mussa Manyanga na Revocatus Mahenge wote wa Parokia ya Bikra Maria wa Fatima Geita Mjini, na Yovenary Mihayo wa Parokia teule ya Mt. Martha Ludete.
