Serikali imeiagiza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) zatakiwa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya katika jamii.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alipofanya ziara ya kikazi katika taasisi hiyo ili kuelewa utekelezaji wa majukumu ya TET katika kukuza sekta ya elimu nchini.
Wanu amepongeza juhudi za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mitaala iliyoboreshwa, akibainisha kuwa hatua hizo zinaonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ubora wa elimu.
Aidha, ameiomba taasisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo, hususan katika kuandaa maudhui ya ujifunzaji kwa watoto wadogo kupitia katuni zinazozingatia maadili na tamaduni za Kitanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa kushirikiana na wadau ili kutatua changamoto za ufundishaji na ujifunzaji.
Dkt. Komba ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za kutosha zinazowezesha uandishi, uchapaji, na usambazaji wa vitabu katika shule zote nchini kwa wakati.
