Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametambua mchango wa majaji wanawake nchini kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia (GBV), akisisitiza kuwa jukumu lao sasa limevuka kuta za mahakama na kuingia kwenye jamii.
Akizungumza leo, Machi 10, 2026, jijini Dodoma katika kilele cha Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake, Dkt. Homera amebainisha kuwa uwepo wa wanawake katika kiti cha utoaji haki unatoa faraja na tumaini jipya kwa waathirika wa ukatili.
Maadhimisho hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), yameongozwa na kaulimbiu ya “Kutoka katika kuta za Mahakama hadi kwenye Jamii: Majaji Wanawake wakiongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.”
Waziri Homera amempongeza Jaji Mkuu, Mhe. George M. Masaju, na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, kwa kuiongoza mahakama katika mapinduzi ya kidijiti na kwamba matumizi ya teknolojia yameleta matokeo makubwa kupunguza msongamano wa mahabusu nchini.
Dkt. Homera ameeleza kuwa mahabusu na magereza ya Tanzania yana uwezo wa kuhifadhi watu 29,000, lakini kutokana na ufanisi wa mahakama mtandao, idadi hiyo imeshuka hadi takriban 23,000 nchi nzima.
Aidha amesema mpango wa usikilizaji mashauri kwa njia ya mtandao na kuachana na matumizi ya karatasi umeongeza kasi ya upatikanaji wa haki na kupunguza ucheleweshaji wa kesi.
