
Wajumbe wa Marekani na Urusi wanakutana mjini Istanbul leo kwa mazungumzo ya kurejesha shughuli za balozi zao, ambazo zilipunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wafanyakazi kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Shirika la habari la AFP, limeripoti kuwa wajumbe wa Urusi na Marekani wamewasili katika jengo la ubalozi mdogo wa Urusi mjini Istanbul.
Siku ya Jumanne, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tammy Bruce, aliwaambia waandishi habari kwamba pande hizo mbili zitajaribu kuimarisha zaidi shughuli za balozi hizo mbili.
Bruce amesema hakuna masuala ya kisiasa au usalama kwenye ajenda na Ukraine haitajadiliwa kabisa.
Mazungumzo hayo ambayo ni ya pili ya aina yake, yanafanyika baada ya Rais Donald Trump kuwasiliana na Urusi wakati alipoanza muhula wake wa pili madarakani, na kuahidi uhusiano bora zaidi ikiwa Urusi itamaliza mapigano yake nchini Ukraine.