Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda, Simon Masondole amesema maadhimisho ya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, yanapaswa kutumika kama darasa kwa jamii kujifunza uzalendo na uwajibikaji katika ujenzi wa taifa.
Akizungumza leo Machi 17, 2026 katika Uwanja wa JS nyumbani kwa hayati Magufuli wilayani Chato, wakati wa misa ya kumbukizi ya miaka mitano ya kifo chake, Askofu Masondole amesema Mungu huwaendeleza wale wanaotenda mema kwa kuishi katika haki na ukweli.
Amesema hayati Magufuli alionesha mfano wa maisha ya kizalendo kwa kujitoa kikamilifu kulijenga taifa, hususan katika usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo.
“Maadhimisho haya yawe shamba darasa kwa kila mmoja wetu kujifunza namna ya kuwajibika na kuipenda nchi yetu,” amesema Askofu Masondole.
