Viongozi wa Makanisa ya Kikristo ndani ya Baraza la Makanisa la Sudan Kusini (SSCC) wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi katika mkoa wa Jonglei, wakionya kuwa hali ya usalama inaendelea kuwa mbaya na kuhatarisha maisha ya raia wengi.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza hilo, Kardinali Ameyu Martin Mulla amesema kampeni ya kijeshi inayoendelea, hususan awamu ya pili iliyopangwa kufanyika katika mji wa Akobo, inaweza kuongeza mateso kwa wananchi na kusababisha watu wengi zaidi kuyahama makazi yao.
Mji wa Akobo umeendelea kuwa kitovu cha mapigano kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) linalomtii Rais Salva Kiir na kundi la upinzani la SPLA-IO linaloongozwa na Riek Machar, Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya wananchi kuvuka Mto Pibor kuelekea Ethiopia wakitafuta hifadhi.
Kanisa limeonya kuwa kuongezeka kwa mapigano kunahatarisha kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyotokea mwaka 2013, huku likikumbusha kuwa licha ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018, bado mvutano wa kisiasa umeendelea kuwepo nchini humo.
Viongozi hao wa dini wamezitaka pande husika kuacha matumizi ya nguvu na badala yake kuanza mazungumzo ya amani, wakisisitiza umuhimu wa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa akiwemo Riek Machar ili kufanikisha maridhiano na kuleta amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.
