
Uongozi wa kata ya Buseresere wilayani Chato mkoani Geita umesema kuwa umepokea shilingi milioni 900 kwa ajili ya kutatua changamoto ya ubovu wa visima vya maji na madaraja katani humo.
Diwani wa kata ya Buseresere Godfrey Mitti amesema baadhi ya vijiji katika kata hiyo vinategemea huduma ya maji, katika visima ambavyo vimeharibika kutokana na sababu za kimazingira na kwamba fedha hizo zimeenda kutatua kero ya maji moja kwa moja.
Amesema kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji baadhi ya visima tayari vimekarabatiwa na wananchi wameanza kupata huduma ya maji huku baadhi ya barabara zilizokua zimekatika zikijengewa madaraja.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Imwelo katika kata ya Buseresere Hezron Mathayo, Bundara Selemani na Paschali Fransisco wameipongeza serikali na kuomba uongozi wa kata hiyo kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha hizo ili changamoto zilizolengwa zitatuliwe kwa wakati.