Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na matishio ya uhalifu unaovuka mipaka katika Ziwa Victoria.
Akifungua Mkutano wa Sita wa Kikundi Kazi cha Kikanda kuhusu kuimarisha usalama wa mipaka katika Ziwa Victoria, uliofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza leo, Mtanda amesema kuwa changamoto hizo zinahitaji hatua za pamoja kutoka kwa nchi zinazolizunguka ziwa hilo.

Amesema ukubwa wa ziwa hilo pia umeambatana na changamoto za kiusalama ikiwemo biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, silaha pamoja na uvuvi haramu unaoharibu rasilimali za mazingira.
Aidha Mtanda ameeleza k uwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu pamoja na mafunzo maalum kwa zaidi ya maafisa 350 kutoka taasisi za ulinzi na usalama.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji, Polisi wa Majini, Mamlaka za Bandari na Idara za Uvuvi katika kudhibiti uhalifu, kuimarisha doria pamoja na kubaini nyaraka bandia katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Katika mkutano huo pia kumefanyika makabidhiano ya uenyekiti wa Kikundi Kazi cha Kikanda kutoka Uganda kwenda Tanzania, ambapo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania (CGI), Dkt. Anna Makakala, amekabidhiwa rasmi jukumu hilo la kuratibu shughuli za kikundi hicho kwa kipindi kijacho.
Mkutano huo unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) unawakutanisha wajumbe kutoka Tanzania, Kenya na Uganda kujadili mikakati ya pamoja ya kuimarisha usalama wa mipaka, kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka na kulinda rasilimali za Ziwa Victoria kwa manufaa ya wananchi wa ukanda huo.
