Mahakama Kuu ya Tanzania imewahukumu kunyongwa hadi kufa maafisa watatu wa Uhamiaji Fredrick Kyomo, Joachim Trathizius na Mabruki Hatibu, kwa kosa la kumuua Enos Elias, mkazi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, ambaye walidhania kuwa si raia wa Tanzania.
Hukumu hiyo imetolewa Desemba 15, 2025, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Augustine Rwizile, ambapo amesema kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeonesha bila shaka yoyote kuwa hakuna mtu mwingine au kundi lolote lililohusika katika mauaji hayo isipokuwa maafisa hao watatu.
Enos Elias alikamatwa na maafisa hao katika kituo cha ukaguzi cha Kihomoka, Wilaya ya Kakonko, Oktoba 27, 2023, na kupelekwa katika ofisi za Uhamiaji kwa ajili ya mahojiano, na akiwa chini ya ulinzi, aliwasiliana na ndugu zake na kuwaomba walete kadi yake ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Hata hivyo, ndugu hao walipofuatilia suala hilo katika ofisi husika, waliambiwa kuwa Enos Elias aliachiliwa huru Oktoba 28, 2023.
Baada ya hapo hakupatikana tena mpaka pale mwili wake ulipogunduliwa Oktoba 29, 2023.