Kadinali Robert Francis Prevost ndiye kiongozi mpya wa kanisa katoliki duniani akichukua jina la Papa Leo XIV. Papa Mteule huyo alichaguliwa na zaidi ya kura 89 za makadinali 133 waliyokuwa katika mchakato wa kumtafta mrithi wa hayati Papa Francis.

Lakini je, Kadinali Robert Francis Prevost ni nani?
Robert Francis Prevost (69) ni mzaliwa wa Septemba 14, 1955 mjini Chicago, Illinois, USA. Robert ni mtoto wa Louis Marius Prevost, baba mwenye asili ya kifaransa na kiitalia na mama mhispania Mildred Martinez. Alisomea katika seminari ndogo ya mapadre Waagostino kabla ya kuhitimu na shahada ya hisabati katika chuo cha Villanova mwaka 1977.
Robert Francis aliamua kuwa Padre na kujiunga na Shirika la Mapadre Waagostino mwaka huo huo wa 1977. Aliweka nadhiri zake za kwanza mwaka mmoja baadaye kabla ya kuweka nadhiri za maisha katika shirika hilo la Waagostino mwaka 1981.
Robert Francis, kwa sasa Papa Leo XIV alipata daraja ya upadre Juni 19, 1982 mjini Roma Italia. Mwaka 1998, Prevost aliteuliwa mkuu wa Shirika la Mapadre Waagostino na kuhudumia kwa mihula miwili ya miaka sita.
Novemba 3, 2014, hayati Papa Francis alimteua kuwa Mhashamu Askofu na kusimikwa Desemba 12, 2014 katika kanisa kuu la mtakatifu Maria jijini Chicago mwaka mmoja babadaye. Aliteuliwa kuwa Kadinali Septemba 30, 2023. Hayati papa Francis amefanya kazi kwa ukaribu sana na Kadinali Robert Francis Prevost, sasa Papa mteule Leo XIV.
Kadinali Robert Francis Prevost ni Papa wa pili kutoka Shirika la Mapadre Waagostino. Ni Papa wa kwanza kutoka Marekani ya Kaskazini. Anazungumza lugha tano: Kiingereza, Kihispania, Kiitalia, Kifaransa na Kireno na anaweza kusoma lugha ya Kilatino na Kijerumani.