Naveed Akram, mshukiwa aliyenusurika katika shambulio la risasi la Jumapili huko Bondi Beach mjini Sydney, ameshtakiwa kwa makosa 59, kati ya hayo 15 ya mauaji na kitendo cha kigaidi.
Baba yake Sajid Akram, 50, aliuawa katika makabiliano ya risasi na polisi katika eneo la tukio baada ya mmoja wa wananchi kukabiriana naye.
Watu 15 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo lililenga jamii ya Wayahudi ya Australia katika hafla ya kuadhimisha usiku wa kwanza wa Hanukkah.
Akram pia anakabiliwa na mashtaka 40 ya kusababisha madhara makubwa ya mwili kwa nia ya kuua, na shtaka moja la kuonyeshwa hadharani nembo ya shirika la kigaidi lililopigwa marufuku.
Alijeruhiwa vibaya wakati wa tukio hilo Jumapili, na kesi yake ilisikilizwa kwa mara ya kwanza akiwa kitandani hospitalini, kwa mjibu wa mahakama ya New South Wales.