Papa Leo wa XIV ameonesha huzuni kubwa kufuatia vifo vya watu wasio na hatia vilivyosababishwa na mashambulizi ya mabomu katika siku za hivi karibuni Mashariki ya Kati.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu na kusambazwa kupitia chaneli yake ya Telegram, Papa amesema anasikitishwa na vifo vya raia wengi wakiwemo watoto pamoja na watu waliojitolea kuwasaidia majeruhi.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni Padre wa Kanisa la Kikatoliki la Kimaronite, Padre Pierre El-Rahi, aliyeuawa alasiri ya tarehe 9 Machi mwaka huu katika kijiji cha Qlaya nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa Padre Toufic Bou Merhi wa Shirika la Wafransisko, Padre Pierre alikuwa pamoja na vijana kadhaa wakikimbia kwenda kumsaidia muumini wa parokia yao baada ya nyumba moja karibu na kanisa kulipuliwa kwa bomu.
Hata hivyo, wakati wakiwa katika harakati za kutoa msaada, bomu lingine lililipuka katika eneo hilo na kumjeruhi Padre huyo pamoja na muumini mmoja wa parokia.
Majeruhi hao walikimbizwa katika hospitali ya eneo hilo, lakini Padre Pierre alifariki dunia kabla ya kupatiwa matibabu.
Wakati huo huo, mashirika ya kimataifa yanayohusika na haki na ustawi wa watoto, yakiwemo UNICEF na Save the Children, yanasema takribani watoto 300 wamepoteza maisha tangu kuongezeka kwa mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika ujumbe wake, Papa Leo wa Kumi na Nne amesema anaendelea kufuatilia kwa karibu matukio hayo kwa wasiwasi mkubwa na ameomba kusitishwa mara moja kwa mapigano ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia, hususan watoto.
