Baba Mtakatifu Pope Leo XIV ametoa idhini ya kuwaweka wakfu mashemasi nane katika Daraja la Upadre na mafrateri saba daraja la Ushemasi kwa ajili ya Kanisa Katoliki ndani ya Jimbo Kuu la Roma.
Uamuzi huo ulitolewa Machi 7, 2026 baada ya kupokea mapendekezo kutoka tume maalum inayoshughulikia maandalizi ya wanaopandishwa katika Daraja Takatifu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Vikarieti ya Roma, watarajiwa wanane watawekwa wakfu katika Daraja la Upadre Jumamosi Aprili 26, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Sherehe hiyo itafanyika katika Dominika ya Nne ya Pasaka inayojulikana pia kama Dominika ya Mchungaji Mwema. Watakaopokea daraja hilo ni Guglielmo Lapenna, Giorgio Larosa, José Emanuele Nleme Sabate, Giovanni Emanuele Nunziante Salazar, Antonino Ordine, Yordan Camilo Ramos Medina, Daniele Riscica na Cristian Sguazzino.
Aidha, Mafrateri saba watawekwa wakfu Aprili 18, 2026 saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya katika Kanisa Kuu la Papa la Mwokozi Mtakatifu Sana na la Watakatifu Yohane Mbatizaji na Mwinjili. Sherehe hiyo itaongozwa na Makamu wa Papa wa Jimbo Kuu la Roma, Baldassare Reina, kwa tendo la kuwekewa mikono.
Jimbo Kuu la Roma limesema tukio hilo ni la furaha kwa Kanisa na limewaalika waamini wote kuwaombea wanaopokea daraja hilo ili wawe waaminifu kwa wito wao na kuwa watumishi wanyenyekevu na wenye furaha wa Injili kwa moyo wa Kristo.
Vilevile, waamini wamehimizwa kuendelea kuliombea Kanisa ili liweze kupata miito mipya na mitakatifu ya Upadre na Ushemasi, ili Bwana aendelee kulijenga Kanisa lake na kuwapa waumini wachungaji na wahudumu wakarimu.
