Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wameomba wadau wa mazingira na serikali kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya majiko banifu ambayo hayahitaji kuni nyingi ili kukabiliana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.
Magreth Bazibanka na Paskazia Masabo wamesema hayo wakati wakiongea na Redio Kwizera kufuatia mikakati iliyowekwa na serikali pamoja na shirika la mpango wa chakula duniani WFP kutoa majiko na elimu ya kutumia majiko banifu.
Wamesema mpango huo utasaidia kutunza mazingira na kupunguza baadhi ya magonjwa yanayotokana na moshi yakiwemo ya macho na kifua.
Bw. Baraka Mkiraha kutoka ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo amesisitiza waliopata majiko hayo kupitia mpango huo, waendelee kuyatumia ili kuongeza hamasa kwa watu wengine kuona umuhimu na faida ya majiko hayo.
