Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso, ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 94.82 ya kura.
Matokeo hayo yametangazwa usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 18, 2026 na televisheni ya taifa hilo. Kwa ushindi huo ushindi huo Nguesso mwenye umri wa miaka 82 ataendeleza utawala wake ambao umechukua takribani miaka 42 katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Katika matokeo hayo, mshindani aliyeshika nafasi ya pili, Mabio Mavoungou Zinga, amepata asilimia 1.48 ya kura.
Vyama vikuu vya upinzani chini humo vilisusia uchaguzi huo, huku baadhi ya vigogo wa upinzani akiwemo Jean-Marie Michel Mokoko na Andre Okombi Salissa wakiwa gerezani kwa takribani muongo mmoja sasa.
Siku ya kupiga kura Jumapili ya March 15, 2026 kuliripotiwa changamoto kadhaa ikiwemo kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura na kukatika kwa huduma ya intaneti nchini kote.
Licha ya hayo, televisheni ya Taifa ilieleza kuwa jumla ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa asilimia 84.65, ingawa katika baadhi ya vituo jijini Brazzaville kulishuhudiwa idadi ndogo ya wapiga kura.
