Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Balozi Ombeni Sefue, amewasilisha uchambuzi mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa mfumo wa sasa wa kodi unawaumiza wananchi na kuwafanya wapoteze imani na serikali.
Balozi Sefue amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti hiyo Machi 18, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, na ameeleza kuwa kero ya kodi nyingi kwenye chanzo kimoja inasababisha wafanyabiashara kuona bora kutoa rushwa ili “kuondoa udhia.”
Amesema mrundikano wa mamlaka za udhibiti kama TRA, na Serikali za Mitaa (LGAs) ambazo zote zinategemea chanzo kimoja cha biashara; kila moja inadai tozo, ada, au ushuru wake bila uratibu, jambo linalosababisha kero na gharama kubwa za uendeshaji biashara.
Tume imebaini kuwepo kwa viwango vikubwa vya kodi na uanzishwaji wa tozo na ada mpya bila uratibu wa malengo mapana ya taifa.
Hali hiyo inasababisha mazingira ya biashara kutotabirika jambo ambalo ni sumu kwa wawekezaji wa ndani na nje, Tume imebaini kuwa walipakodi wamepoteza imani na mifumo iliyopo ya kutatua migogoro ya kodi. Balozi Sefue amesisitiza kuwa wadau wanaona vyombo hivyo havina uhuru wa kutosha kimfumo na kiutendaji, hivyo walipakodi wanahisi hawatendewi haki wanapokuwa na malalamiko dhidi ya Mamlaka ya Mapato (TRA).
Balozi Sefue amebainisha kuwa mazingira haya yanachochea ukwepaji kodi na yanarudisha nyuma juhudi za Rais Samia za kuvutia uwekezaji.
Tume imeshauri kuwepo kwa uratibu wa pamoja wa mamlaka zote zinazokusanya mapato ili kupunguza usumbufu kwa walipakodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji bila kutumia nguvu au vitisho.
