Uongozi wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) umekabidhi rasmi nyaraka za ofisi kwa viongozi wapya wanaoongozwa na Rais Hasheem Thabeet katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Makabidhiano hayo yalisimamiwa na Ofisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu aliyemwakilisha Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha.
Akizungumza Maguzu alisisitiza kuwa viongozi wa vyama vya michezo wanapaswa kukabidhiana ofisi ndani ya muda usiozidi wiki moja ili kuwapa nafasi viongozi wapya kujipanga vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, amesema Rais mpya wa TBF ana jukumu kubwa la kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini, akieleza kuwa uzoefu wake wa kucheza mpira wa kikapu nchini Marekani unaweza kuwa chachu ya kuleta mafanikio makubwa zaidi kwa mchezo huo.

Maguzu pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa michezo, BMT na kamati mbalimbali za michezo pamoja na kuimarisha miundombinu ya viwanja na programu za kuendeleza vipaji kwa watoto ili kuongeza idadi ya wachezaji bora nchini.
Kwa upande wake, Rais mpya wa TBF, Thabeet, amesema anahitaji ushirikiano kutoka Serikalini na kwa viongozi waliomaliza muda wao ili kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya mpira wa kikapu nchini.
Naye Rais wa zamani wa TBF, Michael Kadebe amesema wako tayari kuendelea kushirikiana na uongozi mpya kwa kutoa ushauri na mawazo yatakayosaidia kuendeleza mchezo huo nchini.
