Zaidi ya miti laki tano imepandwa katika Manispaa ya Tabora ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani, hatua inayolenga kuhifadhi mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za asili kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Akiongoza zoezi hilo, Muhifadhi Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Aloyce Kilemwa, amesema miti ina mchango mkubwa katika maisha ya binadamu, ikiwemo kuwa chanzo cha chakula, mbao, kuni, kivuli pamoja na kusaidia kulinda mazingira.
Hata hivyo, Kilemwa amebainisha kuwa changamoto kubwa bado ni utunzaji wa miti inayopandwa, hususan kutokana na baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo katika maeneo ya upandaji, hali inayosababisha uharibifu wa miti na mazingira kwa ujumla.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda miti hiyo ili iweze kukua na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za kisheria wakati wa ukataji miti, ikiwemo kupata vibali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) badala ya kukata kiholela, jambo linalochangia uharibifu wa mazingira.
Kilemwa ameongeza kuwa usimamizi endelevu wa misitu ni nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
