Kenya iko katika hatari ya kupoteza haki ya kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Africa Cup of Nations (AFCON) 2027 baada ya kushindwa kuwasilisha ada ya uenyeji inayokadiriwa kufikia Sh 78.2 Bilioni kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani nchini humo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo, Elijah Mwangi, aliiambia Kamati ya Bunge ya Michezo na Utamaduni kuwa malipo hayo yanapaswa kufanyika ifikapo Machi 30, 2026, chini ya zabuni ya pamoja ya “East Africa Pamoja” inayoshirikisha Kenya, Uganda na Tanzania.
Inaelezwa kuwa Uganda na Tanzania tayari zimeshalipa michango yao, huku Kenya ikiwa bado haijatekeleza wajibu huo. Kushindwa kufikia muda uliowekwa kunaweza kudhoofisha uaminifu wa nchi hiyo kama mwenyeji wa mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Aidha, kumeibuka wasiwasi kuhusu maandalizi ya miundombinu, ambapo viwanja vya Kasarani Stadium na Nyayo Stadium vinatajwa huenda visikamilike kwa wakati kulingana na ratiba ya CAF ndani ya miezi sita ijayo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ukarabati wa Uwanja wa Kasarani umepungua kasi kutokana na deni la takribani Sh 74 bilioni, huku kazi za Uwanja wa Nyayo zikisimama kufuatia madai ya malipo yasiyolipwa ya karibu Sh 54 Bilioni.
