Klabu ya Simba imekata mzizi wa fitina baada ya kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili kiungo mshambuliaji kutoka DR Congo Elie Mpanzu, mapema leo Jumatatu, Machi 23, 2026.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa uvumi mwingi uliokuwa ukiashiria kuwa nyota huyo angeondoka Msimbazi mwishoni mwa msimu huu. Mpanzu, ambaye mkataba wake wa awali wa miaka miwili ulianza Januari 2025 na kutarajiwa kumalizika Desemba 2026, alikuwa ameshaanza kuhusishwa na klabu nyingine kutokana na kusalia na muda mfupi wa mkataba.

Uongozi wa Simba, chini ya mwekezaji wake Mohamed Dewji ‘Mo’, umeingilia kati na kukamilisha dili hilo lililomfanya Mpanzu kuongeza miaka mingine miwili. Kwa makubaliano haya mapya, kiungo huyo sasa atasalia klabuni hapo hadi Desemba 2028.
Kusaini kwa Mpanzu ni pigo kwa timu zilizokuwa zikivizia saini yake na ni habari njema kwa mashabiki wa ‘Wekundu wa Msimbazi’ ambao wamekuwa na hofu ya kumpoteza mchezaji huyo mwenye mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Kukamilika kwa dili hili kunatoa ishara ya dhati ya klabu hiyo kuendelea kuimarisha kikosi chake na kutengeneza utulivu kuelekea msimu ujao wa mashindano.
