
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme, mafuta, na gesi asilia, sekta ya umeme bado inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akizindua taarifa ya maendeleo ya utendaji katika sekta ya nishati kwa mwaka 2023/24.
Amesema kumekuwa na kilio kikubwa ndani ya sekta hiyo kutokana na vyanzo vingi vya maji vinavyotumika kuzalisha umeme kuharibiwa vibaya, hali inayochangia kuendelea kwa changamoto ya upatikanaji wa umeme.
Aidha, amesema upungufu na uchakavu wa miundombinu ya umeme umeendelea kuwa changamoto sugu, na kwamba serikali sasa inafanya marekebisho makubwa ya kimkakati katika miundombinu hiyo.