Samwel Masunzu- Kibondo, KIGOMA
Zaidi ya shilingi mil 594 kimetumika katika ujenzi wa shule mpya 2 za msingi Nyabwai iliyopo katika kijiji cha Kisogwe kata ya Busunzu na shule ya msingi Karundo iliyopo kijiji cha Kichananga kata ya Rugongwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani kwenye shule mama.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hizo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bw. Stephen Janks amesema shule hizo zilianza ujenzi wake kwa nguvu za wananchi ambapo kwa shule ya msingi Nyabwai, wananchi wamechagia mil 5 huku shule ya Karundo wakichangia mil 6.

Mkuu wa wilaya ya Kibondo Kanali Aggrey Magwaza pamoja na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Kibondo Bw. Hamisi Tahiro wamepongeza jitihada za wananchi hao na kwamba kujengwa kwa shule hizo kutapunguza changamoto za watoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Akiweka jiwe la ufunguzi wa shule hizo, Mbunge wa jimbo la Muhambwe na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema serikali imejipanga katika kuhakikisha miundombinu ya shule inaboreshwa sambamba na huduma nyingine zikiwemo za afya.

Akitoa shukurani kwa niaba ya halmashauri, mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Alex Baragomwa amesema madiwani wataendelea kushirikiana katika kusimamia miradi ambayo inaletwa na serikali pamoja na ile inayoanzishwa na kutekelezwa na halmashauri
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi pia ameshiriki upandaji wa miti kwenye shule hizo pamoja na kufanya mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Kigaga kata ya Rugongwe na kukabidhi mabati 80, na Tsh mil 3 kwaajili ya ujenzi wa soko la Kigaga, mashuka 100 ya wagonjwa kwenye kata za Busunzu na Rugongwe sambamba na kuona wagonjwa waliopo hospitali ya wilaya ya Kibondo.

