Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, amewatahadharisha wachimbaji wadogo katika mgodi wa Msasa wilayani Bukombe mkoani Geita kuepuka propaganda za uchochezi wa uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kusambaza taarifa za upotoshaji au kuchochea taharuki atachukuliwa hatua kali za kisheria bila upendeleo.
SACP Jongo ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wachimbaji pamoja na wananchi wa eneo hilo kufuatia kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi katika mitandao ya kijamii kuhusu athari za ajali ya kuporomoka kwa maduara manne katika mgodi wa Msasa ambapo amesema baadhi ya taarifa hizo zimekuwa zikizua hofu na taharuki isiyo ya lazima, hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi badala ya kusambaza uvumi, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia vyanzo rasmi vya habari ili kupata ukweli wa matukio yanayoendelea.

Kamanda Jongo amesema vyombo vya usalama kwa kushirikiana na wataalamu wa migodi vimechukua hatua stahiki kufuatilia kwa kina tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa eneo lililoporomoka ili kubaini kama kuna watu waliokwama au miili katika eneo husika.
Ameongeza kuwa juhudi za uokoaji na tathmini zinaendelea kwa umakini mkubwa, huku akiahidi kuwa taarifa rasmi zitaendelea kutolewa kwa umma kadri uchunguzi unavyoendelea, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

