Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amemwagiza Kaimu mkurugenzi pamoja na maafisa mikopo kuhakikisha vikundi vyote vinavyostahiki mikopo ya asilimia 10 vinaingiziwa fedha zao kwenye akaunti zao haraka ili kuchochea matokeo chanya ya kiuchumi.
Maagizo hayo yametolewa wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoambatana na zoezi la kukabidhi hundi za mikopo Wilayani humo.
Buswelu amesisitiza kuwa hakuna mantiki ya kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi huku fedha zenyewe zikiwa bado hazijawafikia walengwa.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Raymond Kabekenga, amesema kuwa fedha za vikundi tayari zimeingizwa kwenye akaunti, isipokuwa kwa wanachama ambao bado hawajajisajili kwenye huduma za kupokea taarifa za miamala kutoka benki.
Aidha wanavikundi kufika katika benki walizofungua akaunti ili kuthibitisha uwepo wa fedha hizo.
Baadhi ya wanavikundi vya Wanawake na Vijana walieleza kuwa ucheleweshaji wa mikopo hiyo unakwamisha utekelezaji wa shughuli zao za kiuchumi na kusababisha usumbufu usio wa lazima.
Hata hivyo jumla ya Shilingi Milioni 439.7 zimetolewa kwa vikundi 60 Wilayani Tanganyika, ambapo vikundi 30 ni vya Wanawake, 24 vya Vijana na 6 vya watu wenye ulemavu.
