Wakati kukiwa na kilio cha bei za petroli na dizeli kuwa juu, Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.
Waziri Dkt Nchemba ametoa kauli hiyo Leo Jumatano Aprili Mosi, 2026,wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27.
Amesema Serikali imeona bei ya mafuta ilivyopanda na wataweka mikakati ya kukabiliana na mfumuko huo wa bei ili wananchi kupata unafuu wa bei
wakati huo Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amemuagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kukutana na Kamati ya Bunge ya Nishati ili kujadili hali na mwenendo wa kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Zungu ametoa agizo hilo leo wakati akihitisha shughuli za Bunge na kusisitiza kuwa bila upatikanaji wa uhakika wa mafuta, utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo unaweza kukwama.
Hatua hiyo inakuja kutokana na tangazo la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya ya mafuta ambapo kwa Jiji la Dar la Salaam, Petroli imepanda kwa Sh956 kwa lita kutoka Sh2864 Machi hadi Sh3820 Aprili.
Kwa upande wa dizeli, lita moja sasa watanunua kwa Sh3,806 kutoka Sh2,858 ikiwa ni ongezeko la Sh948.
Ongezeko hilo limetokana na athari za mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati ambapo visima, maghala ya kuhifadhia mafuta, viwanda vya kusafisha mafuta na Iran kufunga lango la Hormuzi linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta inayosafirishwa katika masoko mbalimbali.
